Taarifa mpya za mtoto Doreen wa ajali ya Lucky Vincent
Mtoto Doreen Mshana, manusura wa ajali ya Lucky Vincent, ameruhusiwa
kutoka Hospitali na sasa ameungana na wenzake wawili katika nyumba
maalum wanamoishi, Marekani, jimbo la Iowa.
Awali, wanafunzi wengine waliokuwa wakitibiwa katika Hospitali ya Mercy
Hospital, Sioux City, Saidia Awadh na Wilson Tarimo, waliruhusiwa
kutoka hospitali walimokuwa wakitibiwa.
Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu, ameandika katika ukurasa
wake wa facebook na kueleza kuwa sasa Doreen, ameungana na wenzake baada
ya hali yake kuimarika.
Doreen, alibaki hospitali hapo kutokana na majereha makubwa aliyopata
na hivyo kulazimika kufanyiwa upasuaji mkubwa wa uti wa mgongo.
Wanafunzi hao walinusurika katika ajali ya basi la shule ya msingi ya
Lucky Vincent, iliyoua wanafunzi 32, walimu wawili na dereva, Mei 6
mwaka huu, Karatu, Arusha.