Makala: Ubingwa wa Madrid uwe funzo kwa Conte na wenzake
Real Madrid imeweka historia ya kutetea ubingwa wa michuano ya klabu
bingwa barani Ulaya maarufu kama UEFA Champions League ambapo klabu ya
mwisho kuweza kutetea ubingwa wa kombe hilo ilikuwa ni AC Milan mwaka
1990.
Wachezaji wa Real Madrid wakishangilia jana baada ya kuibuka mabingwa wa Kombe la klabu bingwa ulaya
Sambamba na kutetea ubingwa, ni lazima tukumbushane kuwa huku wakali
hao wa Santiago Bernabeu ndio wanashikilia rekodi ya kutwaa taji hilo
mara nyingi zaidi (12) kwenye historia ya michuano hiyo mikubwa kwa
ngazi ya vilabu barani Ulaya.
Mabao manne ya Real Madrid kutoka kwa Cristiano Ronaldo (2), Casemiro
na Asensio yalitosha kabisa kulifunika bao maridadi la Mario Mandzukic
wa Juventus na kunyakua ubingwa kwa jumla ya mabao 4-1 kwenye dimba la
Millenium jijini Cardiff huko nchini Wales.
Kunako usiku wa fainali hiyo ya UEFA, watu mashuhuri duniani katika
tasnia ya soka waliweza kukusanyika kwenye dimba la Millenium ili
kushuhudia kwa macho yao jinsi ambavyo makocha Zinadine Zidane na
Massimiliano Allegri wakitambiana.
Sio ajabu kuona wanamuziki mashuhuri, waigizaji waliotukuka sambamba
na makocha wakubwa duniani wakiwepo majukwaani kutazama mtanange huu
ambao hata mimi ningekuwepo jijini Cardiff nisingekubali unipite.
Licha ya kutazama mpira dakika 90 na kushindwa kuiona japo sura yake
tu, lakini naamini fika mtu kama Antonio Conte asingeweza kukosa kuwepo
dimbani Millenium kuiunga mkono timu yake kipenzi ya Juventus ambayo
aliweza kuipa mafanikio kama mchezaji lakini pia kama kocha.
Kocha wa Chelsea, Antonio Conte
Antonio Conte ambaye ametoka kuipa Chelsea ubingwa wa Uingereza wiki
kadhaa zilizopita alikuwa na kila sababu ya kuwepo uwanjani hapo
kutazama mechi hiyo ukizingatia kuwa London sio mbali na Cardiff, lakini
pia mapenzi yake kwa Juventus ndio yalikuwa sababu kubwa zaidi kwani
hata angekuwa jijini Roma bado angekwea pipa tu.
Unaweza kujiuliza kwanini nimzungumzie Conte tu wakati makocha wengi
walikuwepo uwanjani hapo kushuhudia mechi hiyo ya kusisimua, lakini nna
kila sababu ya kufanya hivyo.
Conte amesajiliwa Chelsea msimu uliopita na katika msimu wake wa
kwanza ameweza kuipa Chelsea ubingwa wa ligi. Msimu uliopita Chelsea
ilikuwa ikipumulia mashine na kumaliza katika nafasi ya kumi na ujio wa
Conte ulikuwa na maana ya kuirudisha timu hiyo kwenye Top 4 tu ili iweze
kucheza michuano ya UEFA msimu unaofata.
Kwa bahati nzuri Conte ameweza kuvuka malengo kutoka kwenye kurudi
Top 4 hadi kuchukua ubingwa kabisa. Chelsea sasa imerudi UEFA sio kwa
kumaliza katika top 4 tu, bali inaingia ikiwa kama bingwa wa Uingereza,
kwahiyo unaweza ukaona uzito wa kumzungumzia Conte na Chelsea yake kwa
wakati huu.
Conte aliambatana na ndugu yake Gianluigi Conte ambaye pia ni mmoja
wa makocha kwenye benchi la ufundi la Chelsea kuishuhudia Juve
ikimenyana na Real Madrid na bila shaka wawili hao watakuwa wameyaona
yaliyojiri. Najua ilikuwa ni siku mbaya sana kwa ndugu hao wawili,
lakini lazima kuna kitu wametoka nacho uwanjani hapo.
Wakati naiangalia Madrid ikiisasambua Juventus kwa mirindimo ya kila
namna, kwa mbali nilikuwa namuwaza Antonio Conte na Chelsea yake ambayo
na yenyewe imeweza kuvisasambua vilabu vya Uingereza msimu huu.
Namuangalia Conte kwa jicho la tatu na najaribu kuwaza nini ambacho
kocha huyo muitaliano atakuwa ameondoka nacho uwanjani hapo lakini kuna
vitu nahisi mimi na yeye tumewaza sawa.
Safu ya Kiungo
Conte bila shaka atakuwa ameiona safu ya kiungo ya Real Madrid ambayo
bila kupepesa kope nathubutu kusema kuwa ndio imeiua Juventus leo
hususani kipindi cha pili.
Kwenye safu hiyo ya kiungo ya Madrid, Conte atakuwa amemuona Modric
anavyozunguka uwanja mzima kama askari wa doria katika harakati za
kuhakikisha waharifu wa Juve wanatulizwa. Katika kumuona Modric, najua
Conte atakuwa amemfananisha na Ngolo Kante ambaye msimu huu naye amekuwa
hashikiki, hivyo kwa hapo Conte hajaona wivu sana.
Wakati akihisi kuwa na yeye anaye Modric kwenye kikosi chake cha
Chelsea, Conte pia atakuwa amewaona Toni Kroos na Casemiro walivyokuwa
wakifanya shughuli pevu pale katikati na bila shaka atakuwa amejiuliza,
Je, Cesc Fabregas, Nemanja Matic au Nathan Chalobah wanaweza kufanya
shughuli waliyoifanya kina Kroos? Mimi sijui.
Ronaldo
Wakati Conte akishuhudia miujiza ya jini Modric ambaye alikuwepo kila
kona ya uwanja, bila shaka atakuwa alikuwa akimuangalia Cristiano
Ronaldo kwa jicho la sitaki nataka. Conte alimuona Ronaldo mwenye njaa
ya kufunga, Ronaldo mwenye uchu wa kufanya jambo ili Madrid yake iweze
kuneemeka.
Bila shaka akili ya Conte kwa haraka haraka ikamuwaza Diego Costa,
halafu papo hapo ikajiuliza je, Costa ana njaa ya kufunga kama ya
Ronaldo? Je, Costa anaweza kuwa na uchu wa kuibeba Chelsea kwenye
michuano ya UEFA msimu ujao kama Ronaldo ninayemuona sasa? Bila shaka
akili yake ilikosa kumpa majibu sahihi ingawa ukweli anaujua mwenyewe.
Marcelo, Dani Alves, Carvajal
Kadri dakika zilivyokuwa zikizidi kwenda, macho ya Conte yalikuwa
hayapumziki yakiangalia huku na huko, kwani licha ya kumuona Modric kila
kona ya uwanja, bado pia aliweza kuwaona vizuri kina Marcelo, Dani
Alves na Carvajal jinsi ambavyo walikuwa wakipanda na kusababisha
mashambulizi licha ya wao kuwa ni mabeki.
Kwa haraka haraka akili ya Conte ikamuwaza Victor Moses na Marcos
Alonso kwenye Chelsea yake huku akijiuliza je, msimu ujao Moses na
Alonso wataweza kufanya mambo yale ayaonayo kutoka kwa Marcelo na
viberenge wenzie? Kadri muda ulivyozidi kwenda, nna uhakika kichwa cha
Conte kilianza kupata mawazo zaidi.
Somo muhimu
Kwa kifupi nnachotaka kusema ni kuwa Conte akiwa ni miongoni mwa
makocha watazamaji waliohudhuria fainali hii atakuwa amejifunza mengi
hususani juu ya nini michuano mikubwa kama ya UEFA inataka.
Conte ameweza kuipa Chelsea ubingwa wa ligi ya Uingereza na sasa
anaingia kwenye kinyang’anyiro cha UEFA huku fainali ya Cardiff ikimpa
picha nzima.
Kwanza kabisa ameona jinsi ambavyo timu kama Real Madrid ina kikosi
kikubwa. Licha ya kujaza wachezaji hatari ndani, lakini benchi lao lina
wachezaji hatari pia kiasi kwamba huoni afadhali ya aliyeingia kutokea
benchi.
Benchi lina watu kama Bale, Morata, Asensio, Nacho, Pepe, James
Rodriguez na wengine lukuki wenye majina makubwa hali ambayo
inadhihirisha kuwa Madrid sio timu ya mchezo mchezo na imestahili kutwaa
ubingwa mara mbili mfululizo.
Kwa kuliona hilo, Conte arudi kwenye kikosi chake atazame kuwa
akishawapanga kina Kante, Hazard, Luiz na Costa ndani, nje anabaki nani
huko benchi? Je, Costa akiumia kuna mtu kama yeye nje?
Swali linaanzia
hapo.
Wakati Benzema akiwa ndani, Morata yupo benchi halafu ukiuliza
utaambiwa ndio Madrid hiyo hiyo inayomtaka Kylian Mbape au Erick
Aubameyang, lakini kwa Conte mbadala wa Costa ni Michy Batshuayi ambaye
bado sio mtu wa kumtegemea aje kukubadilishia matokeo. Nafikiri hilo
Conte ameliona pia.
Kuna mengi ya kuzungumza, lakini Conte hana budi kuichukulia jeuri
hii ya Madrid kama somo kwake na sio kuishia kumfuta machozi Gigi Buffon
kwa kipigo kizito alichopokea.
Conte lazima aelewe Chelsea ina kikosi kidogo sana ambacho baadhi ya wachezaji wakiumia basi mashabiki roho mkononi
Conte lazima aelewe kuwa huko kwenye UEFA ambako alikuwa anakutamani
ni kugumu na kunahitaji wachezaji wenye uwezo unaojibeba wenyewe kabla
ya kubebwa na timu.
Conte lazima aelewe kuwa kabla ya kushona suti kali ya kuvaa kwenye
mechi za UEFA ni lazima awe na wachezaji kaliba ya Marcelo, Ronaldo,
Modric na wengineo ambao wanaweza kufanya miujiza muda wowote wa mchezo
na sio kuishia kutegemea uwezo wa Eden Hazard pekee ambaye kuna muda
unaweza kuhisi kama safu ya ushambuliaji imemsusia yeye pekee huku Costa
akiwa ‘busy’ kuwaadabisha mabeki wanaomkaba.
Conte lazima aelewa kuwa UEFA ni ngumu, asipoingia sokoni kuziwinda
saini za kina Marco Veratti, Raja Nainngolan, Morata, Van de Vidjki na
wengine wa aina hiyo, basi maisha yake yatakuwa magumu sana kwa
kutegemea kikosi kidogo alichonacho kifanye miujiza ilichofanya msimu
huu.
Sio tu kwa Conte, bali timu zote za Uingereza ambazo zinawania
kurudisha heshima kwenye michuano ya UEFA msimu ujao zijifunze kutoka
kwa Zidane na Madrid yake juu ya nini michuano hiyo inataka na sio
kuishia kutuaminisha kwa mdomo kuwa ligi ya Uingereza ndio ligi ngumu
zaidi duniani badala ya kuthibitisha kwa vitendo, Tukutane msimu
ujao!!!.
Post Comment