Header Ads

PropellerAds

Breaking News

Songea: Madiwani wataka fedha kwa wenye VVU

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, wamemuagiza mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Rajab Mtiula kufuatilia malipo ya Sh14 milioni ya posho za kujikimu za watumishi wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU) ambazo wanazidai ili ziweze kuwasaidia kununua chakula bora.

Ombi hilo limetolewa jana Jumamosi kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo wakati wa kikao cha robo ya tatu ya mwaka cha baraza la madiwani.

Madiwani hao wameonyesha kukwazwa na jitihada ambazo zimekua zikigonga mwamba mara kwa mara za watumishi hao kutolipwa posho hizo.

Diwani wa Viti Maalum, Conrada Milinga alisema kwa muda mrefu watumishi ambao ni waathirika na ugonjwa wa Ukimwi hawajalipwa posho zao za kujikimu hivyo kuona kama wananyanyasika.

Alisema kila siku baraza linaelezwa kuwa mikakati imewekwa na watumishi hao watalipwa lakini hakuna utekelezaji wakati watumishi wanaendelea kukabiliwa na matatizo mengi ikiwemo magonjwa nyemelezi.

Akitoa ufafanuzi kuhusu malalamiko hayo, makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Menas Komba alisema kiasi cha Sh 14 milioni kinatakiwa kulipa watumishi walioathirika na ugonjwa wa Ukimwi na kwamba fedha hizo zinatokana na matumizi mengine (OC) lakini halmashauri bado haijazipata.

Alisema wameshalifikisha suala hilo kwenye kamati ya fedha ingawa alisema kwamba wanaoishi na VVU wamesaidiwa kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo ya ufugaji kuku, nguruwe, mbuzi na ng'ombe hivyo bado hawajawaacha bali wanaendelea kuwasaidia.

Taarifa ya halmashauri hiyo imeeleza kuwa watu 613 wamepoteza maisha katika kipindi cha Januari hadi Machi 2017 kutokana na Ukimwi.