Rais wa Korea akamilisha mchakato wa kuishambulia Marekani
Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un
amesema kuwa amekamilisha mchakato wa kupitia mpango wa kufyatua
makombora manne kuelekea katika ardhi ya Guam ya Marekani.
Kwa mujibu wa taarifa ya uamuzi huo
iliyochapishwa na chombo cha habari cha taifa cha nchi hiyo, KCNA, Kim
Jong Un amesema kuwa wameamua kutulia wakisubiri kuona Marekani itafanya
nini kwanza.
Kauli hiyo ya Kim Jong Un imekuja baada
ya Katibu wa Ulinzi wa Marekani, James Mattis kueleza kuwa kama Korea
Kaskazini itathubutu kuishambulia ardhi yoyote ya Marekani basi ‘mchezo
utakuwa umeanza rasmi’.
Kwa mujibu wa KCNA, Kim Jong Un
ameshaufanyia usaili mpango wa kushambulia Guam kwa muda mrefu na kwamba
ameendelea kujadiliana na wataalam wa jeshi la nchi yake.
Rais wa Marekani, Donald Trump amewahi
kukaririwa akimuonya Kim Jong Un kuwa akijaribu kuishambulia Marekani
atashuhudia vitendo vya ‘kipuuzi’ vya Wamarekani dhidi ya nchi yake.
Marekani na Korea Kaskazini wamekuwa
kwenye mgogoro wa muda mrefu kuhusu mpango wa Korea Kaskazini kufanya
majaribio ya mabomu ya kinyuklia.
Korea Kusini ambayo ni hasimu wa Korea
Kaskazini, imesisitiza kuwa nchi yoyote inayotaka kuishambulia Korea
Kaskazini ni lazima ifanye makubaliano nayo kuhusu mpango huo.