Header Ads

PropellerAds

Breaking News

Manji amuomba radhi Rais Magufuli sakata la Coco Beach

Mfanyabiashara maarufu na Diwani wa Mbagala, Yusuf Manji amemuomba radhi Rais John Magufuli kutokana na kesi aliyoifungua akidai kupewa haki ya uwekezaji katika eneo la Coco Beach jijini Dar es Salaam.

Manji ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Quality Group alishinda zabuni iliyotangazwa na Manispaa ya Kinondoni mwaka 2005, kwa ajili ya uwekezaji wa eneo la Coco Beach karibu na Bwalo la Maofisa wa Polisi lililopo Oysterbay.

Akizungumza kupitia taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana, Manji alisema licha ya kampuni yake kupitia kampuni tanzu ya Q-Consult kuingia makubaliano na Manispaa ya Kinondoni Desemba 21, 2007 kulikuwa na ucheleweshaji wa mradi huo.

“Hali hiyo ilisababisha kampuni yetu kutafuta njia ya sheria katika Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi, Desemba 17, 2007 na kufungua kesi ya ardhi namba 334 ya 2009 ambapo baada ya miezi sita Mahakama Kuu iliagiza Manispaa ya Kinondoni kutekeleza ahadi yake,” alisema Manji.

Hata hivyo, alisema baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani alitangaza kusudio la kulifanya eneo hilo kubakia kuwa la matumizi ya wananchi kama lilivyo sasa.

“Kwa kutambua maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Tano tunatii agizo na kuacha eneo hili liendelee kwa matumizi kama ambavyo linatumika sasa,” alisema Manji na kuongeza kuwa:

“Ninaomba radhi binafsi kwa Rais John Magufuli na Serikali yake kwa sintofahamu yoyote iliyojitokeza wakati wa ufuatiliaji wa jambo hili.”

Manji alisema wamewaagiza mawakili wao kujitoa kama wapinzani katika rufaa iliyowekwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kutodai gharama zozote walizoingia au hasara ya mapato kwa kuwa masilahi yao sio halali ukilinganisha na ya wananchi.

“Mwisho Quality Group Limited inatambua na kuunga mkono juhudi zote za Rais Magufuli za kizalendo katika kusimamia rasilimali za nchi yetu,” alisema Manji.

Desemba 5, 2015, Manji alimwandikia barua Rais Magufuli akimweleza usahihi wa mchakato wa zabuni ya kuendeleza Coco Beach.

Pia, katika barua hiyo alimwomba Rais afanye uchunguzi binafsi chini ya ofisi yake ambayo atashirikia nayo.