Header Ads

PropellerAds

Breaking News

Makala: Nikki Mbishi anatamba na muda, ubunifu ni wake?

MIAKA saba sasa imepita tangu tulipokee kwa mikono miwili jina la Rapa Nicas Machuche ‘Nikki Mbishi’ katika mzuki wa Bongo Fleva.
Nikki Mbishi
Mikono yetu na masikio vilihamasika kufanya hivyo mara baada ya kutuletea wimbo ujulikanao kama ‘Play Boy’ ambao alimshirikisha Ben Pol. Wakati huo wote wawili walikuwa chini ya lebo ya M Lab.
Kwa kipindi hicho cha miaka saba Nikki Mbishi ameweza kutuletea albam mbili. Ya kwanza ni Sauti ya Jongoo na ya pili inaitwa Ufunuo, pia ameweza kutoa kanda mseto (mix tap) moja ‘Malcom XI’.
Kwa kazi hizi, anayohaki ya kuitwa mwana hip hop mpambanaji, hajaishia kuchana tu na kwenda studio kurekodi, alama anayoacha msanii katika muziki wake ni albam, Nikki amefanikiwa kwenye hilo.
Jambo la pili ambalo naweza kujivunia kutoka kwa Nikki Mbishi ni namna anavyotunga nyimbo zake kwa kuangalia baadhi ya mambo ambayo yanapewa nafasi kwa wakati husika (current issue).
Hili kwake anajua namna ya kuliweka kwa kuzingatia ubunifu wa hali ya juu, twende polepole. Picha linaanza hivi
Miaka mitatu nyuma Nikki Mbishi alikuwa kwenye mvutano mkali wa kimaneno na msanii Nay wa Mitego. Kila mmoja alikuwa akirusha ‘vijembe’ kwa mwenzake wa wakati wake. Kwenye hilo Nikki Mbishi aliamua kwenda mbali zaidi na kuingia studio na kurekodi wimbo maalumu kwa ajili ya mvutano huo ambao ulikuwa umeshika kasi katika vyombo vya habari na hata mitandao ya kijamii.
Aliamua kutumia fursa hiyo kwa kuachia wimbo uitwao ‘Neema wa Mitego’. Wimbo huu uliokuwa umejaa mafumbo kibao, uliaminika ulikuwa mahsusi kwa ajili ya Nay wa Mitego lakini hakuna aliweza kuthibitisha hilo kwa kuwa hakuna sehemu aliyokuwa ametajwa. Kwa nini watu wahisi aliyelengwa ni Nay wa Mitego, kwa nini asiwe ni msanii mwingine?. Jibu ni kwamba Nikki alikuwa katika wakati wake wa kujidai. Ni muda pekee ulioaminisha watu kuwa ule wimbo ulikuwa mahsusi kwa Nay wa Mitengo.
Ndiyo, kwa nini wasiamini hivyo ikiwa kila siku wanapishana kauli, sawa tuliamini hivyo lakini hatuwezi kuthibitisha hilo. Nikki Mbishi anatuacha na maswali yetu kutokana na ubunifu aliotumia kuandika wimbo huo. Na kuanza hapo ikawa ndio mtindo wake wa maisha katika muziki wa Bongo Fleva.
Unaujua wimbo wake uitwao Babu Bomba?, kama unajua chukua na hii. Wakati kipindi cha Bibi Bomba kilichokuwa kinaruka Clouds TV kikifanya vizuri ndipo Nikki Mbishi alipotumia muda huo kuachia huo wimbo, kama mtu akija kuusikiliza miaka 10 ijayo anaweza asiuelewe kutokana ubunifu wake/maudhuli ulilenga kipidi fulani. Kweli anaanisha? Ni swali unaloweza kujiuliza pindi utakupowa unasikiliza baadhi ya nyimbo zake. Nilipata shida sana kumuelewa pindi alipotoa wimbo uitwao A.K.A, ilinichukua muda kumuelewa lakini hilo sio mada ya leo tuliweke pembeni.
Mwisho mwaka jana alitoa wimbo uitwao ‘Babu Talent’. Inavyoaminika na wengi wimbo huu ulimlenga kiongozi mmoja wa kundi fulani muziki hapa nchini. Kwa namna alivyotumia lugha ya sanaa kumzungumzia na kumchambua unapata picha halisi ya mtu anayemuimba, lakini ni kweli anamaanisha yeye?. Licha kutaja hadi eneo analotoka huwezi kuthibitisha iwapo ni yeye na ndio maana hakuna aliyejitokeza kumlalamikia Nikki. Tupa hilo kule, leta dili nyingine.
Dili lingine naloweza kukupa ni kuhusu wimbo wa ‘I’m Sorry JK’ ambao ulimuingiza ‘matatani’ mara baada ya kutakiwa na Baraza la Sanaa Taifa (BASATA) kujieleza kuhusu wimbo huo. Sitaki kuingia sana ndani kwenye hili, ila jifunze kitu. Nikki Mbishi amecheza na alama za nyakati (muda) kama makala haya yanavyoeleza mwanzoni. Nikki Mbishi ameangalia ugumu wa maisha wa sasa unaosababishwa na mzunguko wa fedha kuwa mdogo na kugundua ni afadhali kipindi kile cha utawala wanne uliokuwa chini ya Rais Mstaafu Jakaya Kikwete.
Amewazidi wenzake
Nilisoma makala moja aliyoandika mchambuzi wa michezo maarufu nchini, Edo Kumwembe. Mchambuzi huyu alimsifia msanii Darassa kwa kitendo chake cha kumtaja mshambuliaji wa Tanzania Mbwana Samatta anayekipiga katika klabu ya KRC Genk nchini Ubelgiji. Edo alitaja kitendo hiki kama mfano wa uzalendo na kupenda kusifia vya kwetu, pia alihoji kama kulikuwa na ulazima wa msanii Diamond Platnumz kumtaja mashambuliaji wa klab ya Real Madrid na raia wa Ureno, Christian Ronaldo katika wimbo wake wa ‘Nana’. Tupunguze mwendo.
Hata hivyo Diamond alikuja kurekebisha kosa hilo katika wimbo wa Kokoro aliyoshirikishwa na msanii mwenzake kutoka lebo ya WCB, Rich Mavoco. Binafsi nilitemgemea kuona msanii yeyote atakaye jitokeza kuandaka wimbo maalum kwa ajili ya wanamichezo wanaofanya vizuri na kuwakilisha nchi nje kama Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu na Hasheem Thabeet. Nikki Mbishi ameweza kuvunja mpaka huo kwa kutumia silaha zake mbili ambazo ni ‘Muda na Ubunifu. Narudi kusema tena Nikki Mbishi ameweza hilo, kwani hujasikia wimbo wake uitwao ‘Sam Magoli?.
Ndiyo, ni Sam Magoli wala sijakosea, Nikki Mbishi ametoa wimbo akimuelezea Mbwana Samatta alivyolishika soka la Tanzania, wakati huo huo Nikki akijifananisha na mchezaji huyo kwa upande wa hip hop kwa hapa Bongo.
Ni vitu ambavyo ni vigumu kuvifikiria kwa haraka, lakini kwa Nikki vinaonekana kuwa rahisi kutokana na ubunifu wake. Wimbo huu angetoa miaka miwili nyuma pengine hata nisingeandika ujumbe huu, lakini sasa nina kila sababu ya kufanya hivyo kutokana na umarufu alionao MbwanaSamatta kwa sasa. Hapa ndipo linakuja suala la muda nililoeleza hapo awali.
Hili ni faida kwake kwani utachukua mashabiki wake wa siku zote na wale ambao ni wa Mbwana Samatta (wapenzi wa soka) ambao pengine si wapenzi sana wa muziki, lakini hili huenda likawashawishi kuingia na upande huu pia.
Kwa nini Leo Nikki Mbishi
Bila shaka unajiuliza kwa nini niandika kuhusu Nikki, pumzika wale usiwe na shaka. Narudia tena, pumzika usiwe na shaka, siku chache zilizopita Nikki Mbishi ametoa wimbo mpya uitwao ‘Dada Pumzisha Mwili Wako’. Katika wimbo huu anaelezea jinsi wadada wengi wanaharibu miili yao kwa kutumia vipodozi vikali. Hili limekuwa ni tatizo kwa siku za hivi karibuni, kila mara tunashuhudia Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) wakiteketeza vipodozi vya aina hiyo na kutoa elimu kuhusu jambo lakini watu bado hawasikii.
Ni jana tu msanii mwingine, Nikki wa Pili alikaririwa akisema kujichubua ni jambo hatari na baya sasa, yeye alilifananisha na ubaguzi wa rangi. Sasa Nikki Mbishi kwa kujua suala hilo ni Current issue kwa sasa anaamua kutumia ubunifu wake, kisha anachora mashairi na kusema ‘Dada Pumzisha Mwili Wako’, hakuna haja tena ya kukimbizana na vipodozi vyenye kemikali.