Header Ads

PropellerAds

Breaking News

VIDEO: Taarifa aliyoipokea Waziri mkuu Majaliwa kuhusu Faru John


December 6, 2016 akiwa ziarani mkoani Arusha, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliuagiza uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), umletee nyaraka zote zilizotumika kumhamisha faru maarufu kwa jina la ‘John’ kutoka kwenye hifadhi hiyo ifikapo Alhamisi, December 8.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo alipotembelea ofisi za makao makuu ya NCAA zilizoko wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha na kuzungumza na watumishi wa mamlaka hiyo pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafugaji ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.
Leo December 9 2016 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amepokea taarifa inayoelezea utaratibu uliotumika kumhamisha faru John kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Sasakwa Black Rhino Sanctuary iliyoko kwenye Hifadhi ya Grumeti.
Akizungumza katika kikao kilichofanyika nyumbani kwake Oysterbay leo mchana (Ijumaa, Desemba 9, 2016) na kuhudhuriwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe na baadhi ya watendaji wa wizara yake, Waziri Mkuu amesema taarifa hiyo itafanyiwa kazi na wataalamu wa ofisi yake.
‘Nilipokea taarifa yenu jana saa 7 usiku lakini nikaahidi kuwa leo tukimaliza sherehe za maadhimisho ya Uhuru tukutane na kujadiliana kuhusu taarifa yenu’-Waziri Mkuu Majaliwa
Akisoma taarifa hiyo mbele ya Waziri Mkuu, Prof. Maghembe alisema hadi kufikia Desemba 2015 wakati faru John anahamishwa alikuwa na watoto 26 (sawa na asilimia 70.2) ya faru wote waliokuwepo ndani ya kreta.
‘Kati ya faru 37 waliokuwepo ndani ya kreta, watoto wake walikuwa 26 sawa na asilimia 70.2. Uamuzi wa kumuondoa John ulikuwa ni muhimu ili kuwezesha kuongezeka kwa faru weusi na kupunguza tatizo la ‘inbreeding’ ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro’;–Waziri Maghembe.
Baada ya kuhamishiwa Sasakwa, Waziri Maghembe alisema Julai 10, 2016 afya ya faru John ilianza kudorora na alikufa tarehe 18 Agosti, mwaka huu. Taarifa hiyo iliandaliwa na Kamati ya Taifa ya Kuwalinda Tembo na Faru.
Akikabidhi pembe za faru huyo mbele ya Waziri Mkuu, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Kupambana na Ujangili wa Wanyamapori, Robert Mande alimweleza kwamba pembe kubwa ya faru John ilikuwa na uzito wa kilo 3.6 na pembe ndogo ilikuwa na uzito wa kilo 2.3.