Askari anayejiita Faru John ameripoti Kituo Kikuu cha Polisi cha Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam alikohojiwa na kuruhusiwa kuondoka akaendelee
na kazi.
Kuripoti kwa askari huyo kunatokana na agizo alilolitoa jana Jumapili,
Kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa kwa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Temeke, Peter Sima awe amempeleka leo Jumatatu baada ya kutuhumiwa
na wananchi wa Mbagala kwamba amekuwa akidai rushwa.
Kamanda Mambosasa pia ametoa wiki moja kwa Kaimu Kamanda Sima awe
amefuatilia tuhuma za rushwa zilizowasilishwa kwake na wananchi.
Amesema askari huyo ataendelea kufuatiliwa ili kubaini ukweli wa tuhuma
zilizotolewa dhidi yake na endapo zitathibitishwa taarifa zitawasilishwa
kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Simon Sirro na atachukuliwa hatua za
kisheria.
“Kaimu kamanda wa polisi Mkoa wa Temeke alimleta huyu askari ambaye
nimemuhoji na kumruhusu kuendelea na kazi wakati akiendelea kuchunguzwa
ndani ya wiki moja,” amesema Kamanda Mambosasa.
Akizungumza na wakazi wa Mbagala, walilalamika wakidai askari huyo
anayejiita Faru John amekuwa akiwakamata wafanyabiashara na kudai kwa
nguvu rushwa ya Sh20,000.
Wananchi hao wamelalamika kuwa, mfanyabiashara ambaye hatoi fedha hizo
hufungwa pingu na kuzungushwa usiku kucha akiwa kwenye gari la polisi.
Kamanda Mambosasa aliyekuwa akisikiliza kero za wananchi wa Mbagala
Zakhem alisema Jeshi la Polisi haliwezi kuwa na askari anayejipa jina la
mzaha, huku akiwakandamiza wananchi.
Chanzo: Mwananchi