Abiria aliyetamka ‘Allah Akbar’ asababisha ndege kuchelewa kuondoka airport
Abiria tisa wamezua taharuki kwenye kiwanja cha ndege cha kimataifa cha
Zaventem, nchini Ubelgiji baada ya mmoja wao kutamka matamshi
yaliyosikika ‘Allah Akbar’ kwa sauti kubwa mara kadhaa.
Watu hao tisa walitolewa na maaskari kwenye ndege ya shirika
la Ryanair, na kuamriwa mizigo yao kutolewa kwenye ndege ili kukaguliwa
zikiwa zimebakia dakika 10 kabla ya ndegehiyo kuondoka.
Ndege hiyo ililazimika kuchelewa kwa masaa manne ikipisha ukaguzi wa
mizigo ya watu hao, ambao walitambuliwa kuwa ni raia wa Ubelgiji.
Polisi mjini Brussels wamethibitisha taarifa hizo kupitia kituo cha
Runinga cha VTM Nieuws kwa kusema kuwa ni kweli tukio hilo limetokea
siku ya Jumamosi Tarehe 2 Septemba ambapo wavulana hao tisa walikuwa
wanasafiri kutoka Mjini Brussels kwenda Madrid, Hispania.
“Tumepokea taarifa hizo za wanaume tisa waliokuwa wakisafiri
kutoka Ubelgiji kwenda Madrid, Hispania lakini walipoingia kwenye ndege
mmoja wao akaanza kutamka kwa sauti ‘Allah Akbar’ akimaanisha ‘Mungu
mkubwa’ kama mara sita hivi ndipo askari wa usalama wakamtoa kwenye
ndege pamoja na wenzake wote kwa ukaguzi”,amesema Peter De Waele msemaji wa jeshi la Polisi mjini Brussels .
Kwa mujibu wa taarifa kutoka gazeti la TOP 24 abiria
walioshuhudia tukio hilo wamesema lilitokea baada ya ndege hiyo
kuchelewa masaa matatu kuruka na ndipo mtu huyo akaanza utani akitamka
‘Allah Akbar’ huku akicheka.
Hata hivyo abiria hao nane walirudishwa kwenye ndege baada ya ukaguzi
kufanyika na ndege kuendelea na safari yake, ingawaje mpaka sasa bado
haijawekwa wazi sababu za kupekuliwa kwa watu hao kwa mara ya mbili huku
mitandao mingi duniani ikiandika kuwa ni hofu ya ugaidi iliyotanda
nchini Ubelgiji.