Kikongwe ajichora Tatuu za Mourinho mwili mzima
Shabiki wa soka, Vivien Bodycote,
59, ameamua moyo wake ufanye kazi mbili kwa wakati mmoja, kwanza ni
kusukuma damu, pili ni kuhifadhi upendo wake kwa Kocha wa Manchester
United, Jose Mourinho.
Inawezekana hilo likawashangaza wengi lakini ukweli ndiyo huo kuwa
Vivien ni shabiki mkubwa wa kocha huyo raia wa Ureno ambaye pia ni baba
wa watoto wawili.
Vivien hajaficha hisia zake, bali ameziweka wazi kiasi kwamba hata
mumewe, Tony ambaye ana umri wa miaka 76, anafahamu jinsi mkewe
anavyomkubali kocha huyo na ndiyo maana wawili hao wametumia zaidi ya
pauni 800 (Sh milioni 2.3) kuchora tatuu zenye taswira au zinazohusiana
na kocha huyo.
Akielezea zaidi, Vivien anasema: “Huwa ni nadra kwangu kwenda mjini
kisha nirejee nikiwa sina tatuu ya Jose mwilini mwangu, nina tatuu 20
zinazomhusu yeye. Siyo kwamba ni mtu muhimu, ni mtu wa kipekee kwangu.
“Nitafurahi sana nikikutana naye, nipo tayari hata kumsaliti mume wangu
linapokuja suala la Mourinho. Ni mtu mwenye mwonekano wa tofauti, kila
mara ninapofunua gazeti na kumuona huwa napata washawasha kwenye magoti.
“Bei za tatuu zangu zipo tofauti, kuna ambazo nilichora kwa gharama
ndogo ya pauni 60 (Sh 171,850) lakini nyingi ni za pauni 250 (Sh
716,040). Kwa jumla zimenigharimu kama pauni 800.”
Vivien ambaye ni mkazi wa mtaa wa Hinckley Kitongoji cha Leicestershire
hajawahi kwenda uwanjani tangu alipofanya hivyo miaka ya 1900, alipoenda
akiwa na baba yake ambaye kwa sasa ni marehemu lakini hiyo haijamzuia
kuwa shabiki mkubwa wa soka.
Shabiki huyo ambaye umri umemtupa mkono ni bibi mwenye wajukuu, alifunga
ndoa na mume wake wa sasa miaka 15 iliyopita, ameongeza: “Hakuna siku
ambayo inapita bila mimi kuitazama picha ya Jose mtandaoni, nimeathirika
kwa Jose Mourinho.
“Nimekuwa nikiulizwa na majirani kuwa kwa nini nisiwe shabiki wa
Leicester lakini mimi ambacho ninawajibu ni kuwa nipo kwenye penzi zito
na kocha huyo wa soka.
“Kama akiamua kuondoka Manchester United kwenda nje ya nchi kufundisha
hata mimi pia nitaacha kushabikia soka la Uingereza, nitamfuata huko
atakapokwenda.
“Mjukuu wangu aliponiambia wakati Jose alipofukuzwa Chelsea, nilifuta
sherehe zote za Krisimasi na hakukuwa na mlo wa usiku kipindi hicho,
nilitamani kukutana naye na nimweleze hisia zangu jinsi nilivyoumia,
nimpoze.”
Ajabu ni kuwe, mume wa Vivien ndiye ambaye amekuwa akitoa fedha ili
mkewe akajichore tatuu hizo za Mourinho kutimiza furaha yake.
Akizungumzia hali hiyo, Tony anasema: “Anafanya anachopenda huwa sijali
kuhusu kumuongezea fedha au kumpa fedha za kujichora tatuu, najua zina
gharama kubwa lakini sijui gharama yake halisi.
“Sijawahi kupenda mpira na wala siyo shabiki wa mchezo huo lakini miaka
michache iliyopita ndipo nilipoanza kufuatilia kidogo japokuwa sikuwahi
kwenda uwanjani, lakini yeye (mkewe) anapenda.”
Upande wa bibi mwenyewe anasisitiza kwa kusema: “Nimekuwa sifikirii
idadi ya tatuu nilizonazo kwa kuwa kila ninapomaliza kuchora moja huwa
nafikiria nyingine. Tony huwa ananipeleka sehemu za kuchorea na
kuniacha.”
Kuna tatuu ambayo ameiandika Mrs Mourinho akimaanisha yeye ndiye mke wa
Mourinho kisha pembeni yake kuna tatuu ya sura ya Mreno huyo.