Header Ads

PropellerAds

Breaking News

MAJALIWA – JESHI LA POLISI LIFANYE UCHUNGUZI JUU YA MIILI YA WATU ILIYOPATIKANA MTO RUVU


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Polisi kufanya upelelezi kuwabaini waliohusika na mauaji ya watu saba ambao miili yao iliokotwa pembezoni mwa mto Ruvu wilayani Bagamoyo, mkoa wa Pwani, ikiwa kwenye mifuko ya sandarusi, ili hatua kali zichukuliwe dhidi yao.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema serikali imepokea kwa huzuni kubwa taarifa ya kuokotwa kwa miili hiyo Desemba 8, mwaka huu na kueleza kuwa matukio kama hayo, likiwemo la mjasiriamali kuuawa baada ya kutekwa mkoani Tabora, hayavumiliki wala kukubalika.

Alitoa maagizo hayo jana katika Baraza la Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W) lililofanyika kitaifa kijijini Shelui wilayani Iramba mkoani Singida. Waziri Mkuu Majaliwa alikuwa mgeni rasmi.
Alisema, “Serikali kwa kushirikiana na Polisi, tena Waziri wa Mambo ya Ndani uko hapa (akimzungumzia Mwigulu Nchemba aliyekuwepo katika baraza hilo), tutaendelea na upelelezi ili wahusika wachukuliwe hatua kali.”
Jana akihojiwa katika kituo cha televisheni cha Star TV, Mwigulu alisema uchunguzi umebaini kuwa miili saba iliyookotwa Bagamoyo ni ya wahamiaji haramu.
Miili ya watu sita ilikutwa Desemba 7, mwaka huu kando ya mto Ruvu wilayani Bagamoyo ndani ya mifuko ya sandarusi na ikiwa imewekwa mawe ili isielee kisha mifuko hiyo kushonwa kama mzigo wa mazao na kutupwa mtoni. Mwili mwingine uliokotwa Desemba 9, eneo hilo hilo na pamoja na kutokuwa katika mfuko wa sarandusi, ulikuwa umevuliwa shati na kuonekana na majeraha mgongoni na kwenye ubavu umekatwa na kitu chenye ncha kali.
Mwishoni mwa wiki, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Boniventure Mushongi alisema miili yote ilizikwa kwa kuwa ilikuwa vigumu kuwatambua kutokana na kuharibika vibaya huku kukiwa hakuna kitambulisho chochote kinachoashiria watu hao ni nani na wametoka wapi na kwamba Polisi inaendelea na upelelezi kubaini waliohusika na mauaji hayo na atakayebainika sheria itachukua mkondo wake.
Aidha, Waziri Mkuu alisema serikali ipo macho kukabiliana na tishio lolote la usalama na vyombo vya usalama vipo tayari muda na wakati wote. Aliwataka wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama kutoa taarifa wanapoona kuna hatari kwani viongozi wa dini na waumini wa dini hizo ndio walinzi wa Taifa.