LOWASSA – VIKAO VYA NDANI NI VIZURI KULIKO MIKUTANO YA HADHARA
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ameishukuru Serikali kwa uamuzi wake wa kuruhusu vikao vya ndani, akisema “ni vitamu kuliko vya nje”. Lowassa alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya madiwani, viongozi na wabunge wa Chadema mkoani Dar es Salaam. Mafunzo hayo yanaendeshwa na chama hicho kwa kushirikiana na Taasisi ya Konard Adenauer Shiftung (Kas) ya Ujerumani.
Rais John Magufuli alipiga marufuku mikutano na maandamano ya kisiasa, akisema wapinzani wajiandae kwa ushindani wakati wa Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2020 na Jeshi la Polisi likatekeleza amri hiyo, likizuia kwa kusema inahatarisha amani, inalenga kushawishi wananchi kutotii maagizo ya Serikali na wakati fulani polisi ilitumia ugonjwa ulioua watu sita mkoani Dodoma kuzuia hafla ya Chadema. Vyama vya upinzani vimepinga kwa nguvu amri hiyo, vikisema inakiuka katiba ya nchi, Sheria ya Vyama vya Siasa na Kanuni za Vyama vya Siasa. Hata hivyo, Serikali imelegeza zuio hilo kwa kuruhusu mikutano ya ndani na ya wabunge kwenye maeneo yao.