Diamond akiri mtoto wa Hamisa Mobeto ni wa kwake
Msanii wa Bongo Flava, Diamond Platnumz amekiri kumtambua mtoto AbdulLatif aliyezaa na mwanamitindo Hamisa Mobeto.
Akiongea katika kipindi cha Leo Tena ya Clouds FM, msanii huyo
ameweka bayana ya kuwahi kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mrembo huyo
na mtoto AbdulLatif ni wake ila walikuwa na makubaliano ya kutotangaza
katika mitandao.
“Nilifahamiana na Hamisa kabla ya kuwa Miss XXL kipindi kile mwaka
2009 -2010 nilikuwa na mahusiano naye kisha tukaja kuachana. Baada ya
kuachana wakati, mimi nikaendelea na maisha yangu na mpaka naanzisha
mahusiano yangu na Zari. Shetani akanipitia na tukaanza tena kuwa na
mawasiliano ya kimahaba mpaka pale alipopata ujauzito. Nilimuambia mimi
ni Baba mwenye familia yangu. Inabidi jambo hili libaki kati yangu mimi
na wewe. Sikupenda kuikana Mimba, ni damu yangu na kila siku iendayo kwa
Mungu nilikuwa nampatia matumizi,” ameeleza Diamond.
Pia akaongeza kuwa amekuwa akimuhudumia mrembo huyo kutokana na
ujauzito huo kwa kuwa anampatia pesa na kumnunulia gari aina ya Rav4.
“Kabla ya mtoto kuzaliwa nilitoa shilingi milioni. 7 na laki 5 na
nikampeleka hospital ya Private kwa ajili ya kujifungua. Wakati nipo
Uingereza nilimuomba Mama yangu aende hospital kumuangalia mtoto, lakini
yule mwanamke aliwaita waandishi wakaenda kumrekodi na kumdhalilisha
mama yangu,” ameongeza Diamond.
Amesisitiza “Niliporudi kutoka Uingereza nilienda kumuona mwanangu na
nikakaa naye sana. Hakuna wakati wowote ambao nilitengeneza mazingira
ya kumkataa mtoto. Nashangaa kuona kwenye mitandao wanasema nimemkataa
mtoto. Nilichokuwa sitaki ni kuhakikisha mwanamke wangu Zari hatukanwi
kwa kuwa hana kosa lolote.” Pia msanii huyo ameomba radhi kwa familia
yake na mpenzi wake Zari kwa kosa hilo.
Juni 21, mwaka huu kupitia kipindi cha XXL ya Clouds FM, Diamond aliwahi kukana kuhusika na ujauzito wa mrembo huyo na alimtaka amtaje baba halisi wa mimba hiyo.